HISTORIA KABLA YA MAPINDUZI MATUKUFU YA MWAKA 1964.

Kabla ya Mapinduzi ya januari 1964, wananchi walikua hawashirikishwi katika katika maamuzi kuhusu ustawi wa maendeleo yao. Mtiririko wa ngazi za utawala ulikua ni wa kupokea amri na kusimamia utelezaji wa amri hizo ambazo huanzia ngazi ya juu ya utawala na kuteremshwa hadi ngazi ya chini kwa wananchi na jamii kwa ujumla. Maamuzi ambayo hayapigwi wala kujadiliwa na wananchi wa kawaida ila ni utekelezaji tu.

HISTORIA BAADA YA MAPINDUZI MATUKUFU YA MWAKA 1964.

Zanzibar kiutawala iligaiwa katika mikoa mitatu (3), ambapo kisiwa cha Unguja kilikuwa na Mikoa miwili (2) ambayo ni Mkoa wa Mjini ukiongozwa na Mhe. Said Washoto na Mkoa wa Mashamba ukiongozwa na Mtoro Rehani Kingo. Na kwa upande wa Pemba ilikua chini ya Mkoa mmoja ambao uliitwa Mkoa wa Pemba na ukiongozwa na Mhe. Rashidi Abdallah.

Aidha kwa upande wa Kisiwa cha Unguja kulianzishwa Wilaya sita (6) nazo ni Makunduchi, baadae ikawa Wilaya ya Kusini, Chwaka baadae ikawa Wilaya ya Kati, Bubwini baadae ikawa Wilaya ya Kaskazini B, Mkokotoni baadae ikawa Wilaya ya Kaskazini A, Wilaya ya Mjini ilibaki kama ilivyo na Wilaya ya Mfeneshini ikawa Wilaya ya Magharibi.

Majina yote ya Wilaya ndio yalikua Makao Makuu ya Wilaya hizo ambazo kabla ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ndio yalikua makao ya utawala wa mudir. (mudir ni neno lenye asili ya kiarabu ambalo lilitumika kama Wilaya kabla ya Mapinduzi)

Kwa upande wa Kisiwa cha Pemba kulikua na Wilaya 4 ambazo ni Wilaya ya Wete, Wilaya ya Konde, Wilaya ya Chakechake na Wilaya ya Mkoani. Baadae mapema katika miaka ya 70 Wilaya ya Konde ikahamishiwa Wilaya ya Micheweni kwa lengo la kuharakisha ustawi wa maendeleo kwa jamii husika.

Mapema katika miaka ya 70 Pemba iligawanywa katika Mikoa miwili (2), Mkoa wa kaskazini na Mkoa wa Kusini. Nguvu za Utawala katika Mikoa na Wilaya zilikua chini ya uteuzi na maelekezo ya Serikali kuu. Kutokana na kuongezeka kwa wakaazi wa Visiwa hivi sambamba na kuongezeka mahitaji, mfumo wa uendeshaji na shughuli za Chama na Serikali ulibadilika ili kukabiliana na ongezeko hilo.

Mabadiliko ya mfumo wa utawala katika Chama yalilazimisha mabadiliko katika Utawala wa vyombo vya Mikoa, Wilaya, Tawi na Mabalozi wa Nyumba kumi (10) kwa nia ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma zinazostahiki kwa urahisi na uhakika zaidi.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1979 ilipitisha sharia namba 1 kuhusu kamati za Mapinduzi. Kamati hizi za Mapinduzi zilikuwa katika ngazi ya Mikoa, Wilaya na Tawi. Muundo wa uongozi wa kamati hizi haukutofautiana sana na ule uliotangulia mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Katika ngazi za Wilaya na Mikoa kamati za Mapinduzi zilihusika na shughuli kuu zifuatazo.

  • Kutekeleza kazi za Serikali za Mitaa katika maeneo, mitaa na mikoa husika.
  • Kuhakikisha uwepo wa amani na ulizi shirikishi wa raia na mali zao.
  • Kusimamia mipango ya maendeleo na miongozo ya Serikali
  • Kuendeleza siasa ya ujamaa na Mapinduzi katika Mikoa, Wilaya na Matawi.
  • Kuwashirikisha kikamilifu wananchi wote katika mipango ya maendeleo na uchumi kwa lengo la kunyanyua hali za maisha ya wananchi.
  • Kutoa mapendekezo juu ya utekelezaji wa mipango ya Serikali katika Wilaya na Mikoa.

Katika utekelezaji wa kazi zake Mfumo wa kamati za mapinduzi pamoja na mafanikio makubwa uliyoyapata ulijikuta unagongana na dhamana za Wizara na vyombo vyengine vya Serikali.

Katika kuondoa Matatizo hayo, Sharia namba 3 ya mwaka 1981 ilipitishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Sharia ambayo ilitoa mamlaka ya madaraka Mikoani.

Wasiliana nasi


Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ

2277 Barabara ya Vuga,

S.L.P 4220,

70401 Mjini Magharibi,

Tel: +255242230034

Fax: +255242230034

Barua pepe: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Waliotembelea Tovuti

3741780
Today
Yesterday
This Week
This Month
All days
122
170
422
9416
3741780