Chuo cha Mafunzo
Utangulizi
Idara ya Chuo cha Mafunzo ni miongoni mwa Idara tano maalum za Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Nambari 1 ya mwaka 1980 na Sheria Nambari 3 ya marekebisho ya mwaka 2007. Idara inatekeleza majukumu yake chini ya Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ. Aidha, Idara ina jukumu kubwa la kuwapokea wale wote wanaoletwa Chuo cha Mafunzo kwa mujibu wa Sheria, kuwalinda pamoja na kuwarekebisha ili wanaporudi katika jamii wawe raia wema Idara inatekeleza programu mbali mbali zikiwemo fani za Elimu za amali, kazi za mikono, ujenzi, kilimo, ufugaji, ushoni, Uchongaji, Ufundi chuma, Ufundi Magari, Elimu za kujiendeleza pamoja na huduma za ushauri nasaha.
Malengo makuu Ya Idara
- Kutoa huduma bora za Urekebishasji tabia kwa Wanafunzi wa Chuo cha
Mafunzo.
Lengo hili linakusudia kuboresha mazingira kwa kuwapatia zana za kufundishia, pamoja na kujenga uwezo kwa walimu ili kutoa huduma bora za urekebishaji pamoja na huduma za ushuri nasaha kwa wanafunzi wanapoingia na wanapotoka Chuo cha Mafunzo.
- Kusimamia Shughuli za Uongozi na Utawala wa Chuo cha Mafuzo.
Lengo hili linakusudia kuratib shughuli za kiutawala pamoja na usimamizi wa fedha kwa ajili ya kuhudumia shughuli za kiutendaji za Idara.
- Kuboresha shughuli za Uzalishaji
Katika kutekeleza lengo hili Idara inakusudia kuhakikisha inaweka mikakati bora katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na ufugaji, kuboresha mazingira katika fani za amali zikiwemo Ujenzi, Ushoni, Useremala pamoja na kubuni mbinu mpya za uzalishaji na kuongeza mapato kwenye Idara ya Chuo cha Mafunzo.
Dira.
Kuongoza katika kutoa huduma bora za urekebeshaji tabia kwa wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ili watakaporejea katika jamii wawe raia wema.
Dhamira.
Kutoa huduma salama zenye kuzingatia haki, kuongeza ubunifu katika urekebishaji kwa kubuni programu mbali mbali zitakazoweza kuwasaidia wanafunzi kujiendeleza na kujitegemea wanaporejea katika jamii.
Mafanikio Makuu kwa Mwaka 2017/2018
- Huduma za urekebishaji zimetolewa katika fani za Ushoni, Ufundi seremala, Ujenzi pamoja na elimu za watu wazima.
- Watumishi 12 wamejengewa uwezo katika fani mbali mbali.
- Huduma za uendeshaji zimeendelea kutolewa kwa kununua vifaa vya Ofisini, kulipa gharama za mafuta na vilainishaji, huduma za umeme pamoja na matengenezo ya magari na majengo.
- Kuendelea na ujenzi wa jengo la urekebishaji wanafunzi watoto kwa hatua ya ghorofa moja.
- Kupunguza tatizo la maakaazi kwa maafisa na wapiganaji wa Chuo cha Mafunzo kwa kukamilisha ujenzi wa majengo 12 kwa kambini za Kengeja na Tungamaa.
Changamoto
Mabadiliko ya hali ya Nchi yanayopelekea baadhi ya mazao kuharibika ama kukosa kuzalishwa kwa kiwango stahili.
- Uchakavu wa majengo ya wanafunzi na wapiganaji.
- Uhaba wa vitendea kazi kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na uzalishaji.
Njia za Utatuzi
- Kufanya ukarabati wa miundombinu ya kilimo kwa kuweka mfumo wa kisasa wa umwagiliaji.
- Kununua vitendea kazi vya kutosha kwa ajili ya shughuli za urekebishaji, uzalishaji pamoja na shughuli za uendeshaji.
- Kuendelea na ujenzi wa Nyumba za askari na mahanga kwa kambi ya Wete na Kangagani Pemba.