MUUNDO WA MIKOA
Mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, miundo ya Mikoa ilibadilika kwa azma ya kusogeza huduma kwa wananchi. Kiutawala Zanzibar iligaiwa katika mikoa mitatu (3) ambapo Kisiwa cha Unguja kilikua na Mikoa 2 ambayo ni Mkoa wa Mjini ukiongozwa na Mheshimiwa Saidi Washoto na Mkoa wa Shamba ambao ulikua ukiongozwa na Mheshimiwa Suleiman Ameir (Mrembo). Pemba ilikua chini ya Mkoa mmoja ambao uliitwa mkoa wa Pemba ukiongozwa na Mheshimiwa Rashid Abdallah, Aidha kwa upande wa upande wa Unguja kulianzishwa Wilaya sita (6) nazo ni Makunduchi baadae ikawa Wilaya ya Kusini, Chwaka baadae ikawa Wilaya ya Kati. Bumbwini baadae ikawa Wilaya ya Kaskazini B, Mkokotoni baadae ikawa Wilaya ya Kaskazini A. Wilaya ya Mjini ilibaki kama ilivyo na wilaya ya Mfenesini baadae ikawa wilaya ya Magharibi. Majina yote ya Wilaya ndio yalikua makao makuu ya Wilaya hizo ambazo kabla ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 ndio yalikua Makao ya Mudiri.
Kwa upande wa kisiwa cha Pemba kulikua na Wilaya nne ambazo ni: Wilaya ya Wete, Wilaya ya Konde, Wilaya ya Chakechake na Wilaya ya Mkoani. Baadae mapema katika miaka ya 70 Wilaya ya Konde ikahamishiwa Wilaya ya Micheweni kwa lengo la kuharakisha ustawi wa maendeleo ya jamii husika.
Mwanzoni mwa miaka ya 70 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianzisha Mikoa ilianzisha Mikoa Mitano (5) ambayo ni Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkoa wa Kaskazini Pemba na Mkoa wa Kusini Pemba. Kila mkoa ulikua umegawika katika wilaya mbili ili Selikali za Mikoa ziweze kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Sera miongozo na Maagizo ya Serikali kwa karibu zaidi.
Sambamba na mabadiliko hayo, katika mwaka 1998 Serikali ilipitisha sharia Namba 1 ya mwaka 1998 ya Mamlaka ya Serikali za mikoa ambayo ilifafanua zaidi juu ya kazi na majukumu ya wakuu wa Wilaya, pamoja na maofisa Tawala wa Mikoa na Wilaya. Sheria hiyo iliunda kamati za maendeleo za mikoa (Regianal Development Commitees) ambazo zimepewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendelea katika ngazi husika.
Aidha sharia hiyo, imerejesha utawala wa Masheha ambao wanateuliwa na Mkuu wa Mkoa baada ya kushauriana na Mkuu wa Wilaya husika. Kwa mujibu wa sharia hiyo sheha ndio mtendaji mkuu wa Serikali katika ngazi ya chini ya Utawala. Aidha, katika utendaji wake, Sheha huwa anasaidiwa na Baraza la Ushauri wa shehia ambalo linaundwa na wajumbe wasiozidi 12.
Idadi ya shehia zilizopo sasa ni 335 (214 kwa Unguja na 121 kwa Pemba) zilizoanzishwa chini ya sharia hii.
MAJUKUMU YA MAMLAKA YA MIKOA.
Majukumu makuu ya mamlaka za mikoa ni kama yafuatayo;
- Kwa mujibu wa sharia namba 5/1998 ya Tawala za mikoa Zanzibar, Mamlaka za Serikali za mikao zimepewa jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Seriakli katika maeneo ya utawala. Aidha, mamlaka hizo zimepewa jukumu la kutoa miongozo, kutafsiri sera sharia na kuhakikisha uendelevu wa hali ya amani na utulivu katika Mikoa.
- Mikoa ina jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Wilaya na Shehia zilizomo katika Mikoa. Aidha Mikoa ina jukumu la kuhakikisha ulinzi na usalama pamoja na kutatua masuala/matatizo mbalimbali ya wananchi katika Mikoa husika.
- Kuratibu na kusimamia utekelezaji wa malengo ya sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, afya, maji, miundo mbinu, utawala Bora, umeme ustawi wa jamii maendeleo ya vijana ,wanawake na watoto, uvuvi, ufugaji maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
- Kuratibu shughuli mtambuka zikiwemo UKIMWI, jinsia madawa ya kulevya, utawala bora, maswala ya watu wenye ulemavu na mazingira.