Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM)

Baada ya Mapinduzi Matukufu ya 1964, ambayo yaliongozwa na Chama Cha Afro Shirazi Party (ASP) chini ya Jamadari wa Mapinduzi na Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Aman Karume, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianzisha vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo ni JESHI LA UKOMBOZI (JLU), Idara ya Usalama wa Zanzibar na kuimarisha Jeshi la Polisi.

Kikosi cha Wanamaji Zanzibar (Zanzibar Navy) ambacho asili yake ni Idara ya Usalama Zanzibar kilikuwa na malengo ambayo ni kulinda uhuru wa Zanzibar (ambao ulipatikana kwa mapinduzi ya 1964) pamoja na mipaka ya baharini ya Zanzibar na watu wake.
Mnamo tarehe 01/07/1973 Kikosi cha Wanamaji Zanzibar kubadilishwa jina na kuitwa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), mbali ya kubadilishwa jina lakini malengo na madhumuni yake yalibaki kuwa yale yale.
Mwaka 1984 Kikosi cha Wanamaji Zanzibar (Zanzibar Navy) kiliondolewa kutoka Idara ya Usalama Zanzibar na kuwa kikosi kinachojitegemea. Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaeleza kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ndiye Kamanda Mkuu wa kikosi hicho na vyengine vilivyoundwa na vitakavyoundwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Madhumuni ya Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM).
Madhumuni hasa ya kuanzishwa kwa vyombo hivi vya ulinzi na usalama kikiwemo Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo (KMKM) ni kulinda uhuru wa Zanzibar (ambao ulipatikana kwa njia ya mapinduzi ya 1964) pamoja na watu wake na kulinda mipaka ya baharini ya Zanzibar dhidi ya vitisho na wapinga mapinduzi matukufu ya 1964, pia na kuleta ustawi wa wananchi wote wa Zanzibar.

Malengo

Ni kuwa na Kikosi bora na cha kisasa chenye uwezo wa kulinda mipaka ya bahari ya Zanzibar.
Malengo haya yanathibitishwa na kauli ya aliye kuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee. ABEID AMANI KARUME pale alipokuwa akiwaaga vijana wa kundi la kwanza kwa safari ya kwenda mafunzoni nchini Ujerumani Mashariki aliposema
".....Vijana mkasome usiku na mchana maana nchi haina ulinzi wa kutosha baharini"

Kazi za KMKM

Majukumu ya KMKM yameelezwa katika Sheria ya KMKM (Kifungu cha 4(1)(2)(3) cha Sheria ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo), miongoni mwa majukumu hayo ni:
* Kulinda usalama wa bahari ya Zanzibar.
* Kulinda maliasili za bahari.
* Kulinda usalama wa nchi kutokana na majasusi wanaotumia njia za bahari.
* Kuzuia magendo ya aina zote kwa njia zote zinazoweza kutumika kwa kipitishia magendo.
* Kulinda vyombo vya Serikali vinavyosafirisha mali, wananchi, pamoja na viongozi wakati wa vita na hali ya hatari.
* Kusafirisha askari pale inapohitajika.
* Kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika kulinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
* Kupambana na uhalifu unaofanywa kupitia baharini ukiwemo ule wa usafirishaji haramu wa madawa ya kulevya na watekaji nyara.
* Kufanya upekuzi na kufanya shughuli za uokoaji baharini na kulinda mazingira ya bahari.
* Kufanya kazi yoyote itakayotolewa na Rais kwa kuzingatia uwezo, utaalam na nyenzo za KMKM ziliopo.

 

Ushiriki wa KMKM Katika Nyengine Kazi za Kitaifa
Mbali na majukumu hayo KMKM yaliowekwa kisheria, pia KMKM imekuwa ikishiriki kazi kadhaa za kitaifa ikiwemo;-
* Kushiriki kazi za Uokozi wa Mv. Bukoba tukio lilikotokea tarehe 21/05/ 1996 , M.V Spice Island 10 septemba 2011 , M.V Skagit 18 Julai 2012.
* Kutoa huduma za jamii kama matibabu kupitia hospitali yake iliopo Kibweni Zanzibar.
* Kushiriki katika michezo mbali mbali ndani na nje ya nchi kama mpira wa miguu, mpira wa pete, kuogelea, riadha n.k ambayo hufanyika ndani na nje ya nchi na kuliletea taifa sifa njema. Mwaka 1989 KMKM ilichukua ubigwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
* Kutoa elimu ya aina mbali mbali kwa wapiganaji.

 

Kujua zaidi kuhusu KMKM tembelea tovuti yao www.kmkmzanzibar.go.tz

Wasiliana nasi


Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ

2277 Barabara ya Vuga,

S.L.P 4220,

70401 Mjini Magharibi,

Tel: +255242230034

Fax: +255242230034

Barua pepe: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Waliotembelea Tovuti

3752130
Today
Yesterday
This Week
This Month
All days
95
477
2014
7710
3752130