Serikali ya Awamu ya Nane imeendelea kujidhihirisha kwa vitendo katika kuwapatia wananchi maendeleo kupitia ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Barabara ya Mahonda- Pangatupu- Bumbwini (km 11.3) pamoja na Daraja la Pangatupu lenye urefu wa mita 100, Wilaya ya Kaskazini “B”, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema wananchi wana kila sababu ya kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi zake za kuifungua Zanzibar kiuchumi kupitia uwekezaji mkubwa wa miundombinu, sambamba na kulinda Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, amesisitiza kuwa maendeleo lazima yaambatane na amani, umoja na utulivu.