Kuhusu

Sisi ni nani

Historia

Kabla ya Mapinduzi ya Januari 1964, mwananchi walikuwa hawashirikishwi katika maamuzi kuhusu ustawi wa maendeleo yao. Mtiririko wa ngazi za utawala ulikua ni kupokea amri na kusimamia utekelezaji wa amri hizo ambazo huanzia katika ngazi ya juu ya utawala na kuteremshwa hadi ngazi ya chini kwa wananchi na jamii kwa ujumla. Maamuzi ambayo hayapingwi wala kujadiliwa na wananchi wa kawaida ila ni utekelezaji tu. Zanzibar Kiutawala iligaiwa katika Mikoa mitatu ambapo kisiwa cha Unguja kilikuwa na Mikoa miwili (2) ambayo ni Mkoa wa Mjini ukiongozwa na Mh, Saidi Washoto na Mkoa wa Mashamba ukiongozwa na Mtoro Rehani Kingo na upande wa Pemba ilikuwa chini ya mkoa mmoja ambao uliitwa Mkoa wa Pemba ukiongozwa na Mh, Rashid Abdalla. Aidha, kwa upande wa Kisiwa cha Unguja kulianzishwa Wilaya sita nazo ni Makunduchi baadae ikawa Wilaya ya Kusini, Chawaka baadae ikawa Wilaya ya Kati.Bumbwini baadae ikawa Wilaya ya Kaskazini “B.”Mkokotoni baadae ikawa Wilaya Kaskazini “A”, Wilaya ya Mjini ilibaki ilivyo na Wilaya ya Mfenesini baadae ikawa Wilaya ya Magharibi. Majina yote ya Wilaya ndiyo yalikuwa makao makuu ya Wilaya hizo ambazo kabla ya mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 ndio yalikuwa makao ya utawala wa Mudiri. Kwa upande wa Kisiwa cha Pemba kulikuwa na Wilaya nne ambazo ni Wilaya ya Wete, Wilaya ya Konde, Wilaya ya Chake Chake na Wilaya ya Mkoani. Baadae mapema katika miaka ya 1970 Wilaya ya Konde ikahamishiwa Wilaya ya Micheweni kwa lengo la kuharakisha ustawi wa maendeleo ya jamii husika. Mapema katika miaka ya 1970 Pemba iligawanywa katika Mikoa miwili. Mkoa wa Kaskazini na Mkoa wa Kusini. Nguvu za Utawala katika Mikoa na Wilaya zilikuwa chini ya uteuzi na Maelekezo ya Serikali Kuu. Kutokana na kuongezeka kwa wakaazi wa visiwa hivi sambamba na kuongezeka kwa mahitaji, mfumo wa uendeshaji wa shughuli za chama na Serikali ulibadilika ili kumudu kukabialiana na ongezeko hilo. Mabadiliko ya mfumo wa Utawala katika chama yalilazimisha mabadiliko katika utawala wa vyombo cha Mikoa, Wilaya, Tawi na mabalozi wa nyumba kumi (10) kwa nia ya kuhakikisha kwamba mwananchi anapata huduma anazostahili kwa urahisi na uhakika zaidi. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipitisha Sheria Nam.1 ya mwaka 1979 kuhusu KAMATI ZA MAPINDUZI. Kamati hizi za Mapinduzi zilikua katika ngazi ya Mikoa na Wilaya. Muundo wa uongozi wa kamati hizi haukutofautiana sana na ule uliotangulia mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Utekelezaji wa mfumo wa Kamati za Mapinduzi pamoja na mafanikio makubwa uliyoyaleta, ulijikuta unagongana na dhamana za Wizara na vyombo vyengine vya Serikali katika kuondoa matatizo hayo, Sheria Nam.3 ya mwaka 1981 ilipitishwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Sheria ambayo ilitoa mamlaka ya madaraka Mikoani. Mwanzoni mwa miaka ya 70, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilianzisha Mikoa mitano (5) ambayo ni Mkoa wa kaskazini Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkoa wa Kaskazini Pemba na Mkoa wa Kusini Pemba. Kila Mkoa ulikuwa umegawika katika Wilaya mbili, kwa azma ya kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Sera, Miongozo na Maagizo ya Serikali kwa karibu zaidi. Sambamba na mabadiliko hayo, katika mwaka 1998 Serikali ilipitisha Sheria Namba 1 ya mwaka 1998 ya Mamlaka ya Serikali za Mikoa ambayo ilifafanua zaidi juu ya kazi na majukumu ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, pamoja na Maofisa Tawala wa Mikoa na Wilaya. Sheria hiyo iliunda Kamati za Maendeleo za Mikoa (Regional Development Committees) na Wilaya (District Development Committees) ambazo zimepewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika ngazi husika. Aidha Sheria hiyo, imerejesha utawala wa Masheha ambao wanateuliwa na Mkuu wa Mkoa baada ya kushauriana na Mkuu wa Wilaya husika.Kwa mujibu wa Sheria hiyo, Sheha ndie mtendaji Mkuu wa Serikali katika ngazi ya chini ya utawala. Aidha, katika utendaji wake, Sheha huwa anasaidiwa na Baraza la Ushauri la Shehia ambalo linaundwa na wajumbe wasiozidi 12. Kwa hivi sasa Zanzibar ina idadi ya Shehia 388 (259 kwa Unguja na 129 kwa Pemba) ambazo zipo chini ya Sheria hii. Vile vile, zipo Mamlaka za Serikali za Mitaa kumi na moja (11) Unguja zipo saba (7) Pemba zipo nne(4) kati ya hizo Mabaraza ya Manispaa yapo matatu (3) Mabaraza la Manispaa Mjini, Baraza la Manispaa Magharibi “A”,Baraza la Manispaa Magharibi “B” kuna Mabaraza ya miji sita (6) Baraza la Mji Kaskazini A, Baraza la Mji kaskazini B ,Baraza la Mji kati na kwa Pemba yapo matatu (3) Baraza la Mji Mkoani, Baraza la Mji Chakechake na Baraza la Mji Wete na Halmashauri za Wilaya zipo mbili(2) ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Kusini Kwa Unguja na Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni kwa Pemba.

Dira

Kuwa taasisi imara katika kusimamia amani, usalama, usajili wa wakaazi na upatikanaji wa huduma karibu na wananchi

Dhamira

Kujenga mazingira mazuri ya ushiriki wa wananchi katika kudumisha amani, ulinzi wa mali zao, kuimarisha huduma za kijamii, kuhakikisha kuwa jamii inashiriki katika kupanga na kusimamia shughuli za maendeleo katika maeneo yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora ikihusisha kuwatambua wakaazi wa maeneo husika na utambulisho wao.

HUDUMA ZINAZOTOLEWA

  • Kusimamia Sera, Sheria na Kanuni mbali mbali za Ofisi.
  • Kubuni na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo
  • Kudumisha Amani, Ulinzi na Usalama katika Mikoa na Wilaya hadi Shehia.
  • Kulinda mali za Taifa na za watu binafsi zisiharibiwe, kuzuia uingizaji au utoaji nje ya nchi kimagendo, pamoja na kusimamia kazi za uzimaji moto na uokozi.
  • Kuwasajili na kuwapa vitambulisho Wazanzibari wakaazi.
  • Kuwahifadhi kwa kufuata taratibu bora na kwa kuzingatia haki za binaadamu watuhumiwa na waliofungwa ambao wako katika Vyuo vya Mafunzo.
  • Kuandaa na kutekeleza mipango ya kuijengea uwezo Mikoa kitaaluma na utumishi katika Mikoa.
  • Kutoa mwongozo na ushauri kwa Mikoa katika mambo ya kisheria na utaratibu, kujenga mazingira mazuri katika kuimarisha huduma za kijamii na kiuchumi katika Mikoa.
  • Kuratibu, kushauri, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa shughuliza Serikali za Mitaa.
  • Kuimarisha Utawala Bora na kuimarisha uwezo wa Serikali za Mitaa na mamlaka zake.
  • Kufuatilia na kukagua utendaji wa mamlaka za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ katika utoaji wa huduma.
  • Kuendeleza michezo katika Idara na Taasisi zetu.
  • Kuimarisha uhusiano baina ya taasisi za Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ. Na taasisi nyengine

Viongozi

IDRISA KITWANA MUSTAFA

MH WAZIRI OR-TAMISEMIM

Uongozi ni zamana ya muda mfupi tusijisahau tufanye kazi kwa bidii na uaminifu ili kulejenga taifa letu.

ISSA MAHFOUDH HAJI

KATIBU MKUU

Tufanye kazi

MIKIDADI MBAROUK MZEE

NAIBU KATIBU

Tufanye kazi kwa hekma tujenge zanzibar yetu